Thursday, October 25, 2012

VIJANA KATIKA KUPAMBANA NA KIFUA KIKUU NA UKIMWI.

Ugonjwa wa kifua kikuu umekuwepo tangu enzi za mababu wakati UKIMWI umeanza miaka ya karibuni. Hata hivyo inajionyesha waziwazi na tafiti zimedhibitisha kuwa ugonjwa wa kifua kikuu umeongezeka mara dufu baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa UKIMWI.
Taarifa za shirika la afya duniani zinaonyesha kuwa theluthi ya watu wote duniani wana maambukizi ya kifua kikuu na takribani watu milioni nane hupata maambukizi mapya kila mwaka, huku kukiripotiwa kuwa na vifo vya watu milioni mbili kila mwaka.
Taarifa hii anonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maambukizo haya yako katika nchi za Afrika na hasa kusini mwa jangwa la sahara. Tukumbuke kuwa Tanzania iko katika ukanda huu wa kusini mwa jangwa la sahara.
Kifua kikuu kimezidishwa na virusi vya UKIMWI kwa sababu wadudu wa kifua kikuu hushambulia watu wenye upungufu wa kinga mwilini. Virusi vya UKIMWI hushambulia kinga ya mwili na hivyo kutoa nafasi kwa bacteria wa kifua kikuu kuibuka.

Wakati wadudu wa kifua kikuu huingia mwilini kwa njia ya hewa, Virusi vya UKIMWI huingia kwa njia ya kufanya mapenzi bila kinga, kuongezewa damu iliyo na virusi, kuchangia vitu vyenye incha kali na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hata hivyo kuna sababu nyingi sana za kushuka kwa kinga ya mwili ikiwa ni pamoja na lishe duni, magojwa mengine kama malaria, saratani, homa ya matumbo na kadhalika. Napenda kuweka wazi kuwa si kila mwenye kifua kikuu atakuwa na virusi vya UKIMWI au UKIMWI wenyewe.
Kwa hiyo msomaji wangu kuwa huru kufikiria upya kwenda kupima  virusi vya UKIMWI kwani itakusaidia kupona haraka iwapo itagundulika kuwa una virusi vya UKIMWI. Napenda kukumbusha kuwa kifua kikuu ni kati ya magonjwa nyemelezi ya virusi vya UKIMWI kama ilivyo kwa magonjwa ya ngozi, fungus, malaria na kadhalika.
Vijana wa kundi la MUKIKUTE (Mpango wa mapambano dhidi ya Kifua kikuu na UKIMWI Temeke).Kundi hili lilianzishwa mwaka 2008,ambalo mpaka sasa lina washiriki 12.KUndi hili linajihusisha na muziki wa kiasili.Ni vijana ambao wanashirikiana na manispaa ya wilaya ya Temeke katika uhamasishaji na uelimishaji juu ya kifua kikuu na UKIMWI.Wamekuwa wakielimisha jamii kwa njia ya maigizo ya jukwaani pamoja na nyimbo au muziki wa kiasili wanaopiga.Ni mafanikio makubwa yanayoonekana katika wilaya hiyo kutokana na watu wengi kujitokeza katika vituo husika vya afya na kupima afya zao,na kupata elimu zaidi juu ya magonjwa haya hatari ya UKIMWI pamoja na kifua kikuu.Jamii nzima ya watanzania inashauriwa kuhudhuria katika vituo vya afya ili kupata uhakika wa afya zao,na kupata matibabu husika na ushauri nasaha endapo watagundulika kuambukizwa magonjwa haya hatarishi katika nyakati hizi barani Afrika na ulimwenguni kote.

No comments:

Post a Comment